Mbunge wa eneo bunge la Jomvu Badi Twalib ameonya kampuni ya kiwanda cha nguo cha EPZ, dhidi ya kuwanyanyasa wafanyikazi wake.
Akiongea na mwanahabari huyu katika ofisi yake siku ya Jumatano, Badi alidai kuwa wafanyikazi wa kampuni hiyo ya kushona nguo wanafanya kazi masaa mengi bila ya malipo ya ziada, kinyume na sheria na haki za wafanyikazi nchini.
Mbunge huyo alisema kuwa iwapo viongozi wa kampuni hiyo wataendelea kunyanyasa wafanyikazi wake, basi itakuwa wakati mwafaka wa kampuni hizo kufungwa kwa msingi wa kuwadhulumu wafanyikazi.
Badi alisema kuwa hatahimili kuona wananchi wake wakinyanyaswa kwa hali yeyote kinyume na katiba.
Haya yanajiri wakati ambapo wafanyikazi wa kampuni za EPZ wamekuwa wakilalamika na hata kufanya maandamano, kupinga uongozi uliopo katika kampuni hizo.