Mbunge wa Mwea Peter Gitau anaendelea kufanyiwa mahojiano na maafisa wa polisi baada ya kudaiwa kupatika akiwahonga vijana kumpigia kura mgombea wa chama cha Jubilee Philip Charo katika uchaguzi mdogo wa Malindi.
Gitau anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Malindi akisubiri kufikishwa mahakamani kujibu shtaka la kuenda kinyume cha sheria za uchaguzi nchini.
Mbunge huyo wa Mwea ambaye ni mwanachama wa Jubilee anadaiwa kukamatwa na baadhi ya wafuasi wa chama cha ODM, waliotoa ripoti kwa maafisa wa polisi, hatua iliyopelekea mbunge huyo kutiwa mbaroni.
Akizungumza siku ya Jumatatu, Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Kilifi Aisha Jumwa, ambaye pia ni mwanachama wa ODM alidai kumpata Gitau akiwahonga vijana shilingi elfu moja kila moja, ili kubadilisha kura zao.
Jumwa alisema kuwa chama cha Jubilee kinaogopa kushindwa katika uchaguzi huo ndio maana wameanza mbinu ya kuwahonga vijana na akina mama.
"Tumegundua njama ya chama cha Jubilee kuwa inawahonga vijana na akina mama kwa kuwapa shilingi elfu moja kila mmoja, ili kumchangua mfuasi wao wa chama cha Jubilee Philip Charo. Hiyo ni ishara kamili kuwa wamejua ODM itachukua ushindi huu,” alisema Jumwa.