Shahidi wa pili ameiambia mahakama kuwa meli ya MV Amin Darya iliyozamishwa baharini mwaka wa 2014 haikuwa na dawa za kulevya.
Shahidi huyo, Gulam Karima, aliambia mahakama siku ya Alhamisi kuwa aliona mifuko ya saruji pekee, ikitolewa kutoka kwa meli hiyo wala sio dawa za kulevya kama inavyodaiwa.
Ushahidi wake unawiana na ule wa Mkuu wa polisi wa Kituo cha Kilindini Simon Simotwa, aliyeelezea mahakama mwaka jana kuwa ukaguzi wa kwanza wa meli hiyo ulionyesha haikuwa na dawa za kulevya kama inavyodaiwa.
Hata hivyo, ushahidi huu unakinzana na ule wa Athuman Degereko Alfan, ambaye ni afisa wa wanamaji, aliyeiambia mahakama kuwa aligundua meli MV Amin Darya imebeba dawa hizo baada ya kufanyiwa uchunguzi bandarini.
Kesi hiyo inawakabili raia tisa wa kigeni kutoka Pakistan na India, na watatu kutoka Kenya, wanaodaiwa kunaswa na dawa za kulevya bandarini Mombasa zenye thamani ya shilingi bilioni 1.3.
Meli hiyo ilizamishwa baharini na serikali mwezi Agosti 29, 2014 baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutoa agizo la kuchomwa kwa meli hiyo.