Meneja wa kampuni ya usambazaji umeme nchini tawi la Nyamira Dancan Machuka amejitokeza kushtumu wizi wa vikingi vya stima katika kaunti hiyo. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akihutubia wanahabari ofisini mwake siku ya Jumatano, Machuka alisema baadhi ya vikingi vya stima vimekuwa vikiibwa na watu wasiojulikana, hali inayolemaza utoaji huduma kwa wateja. 

"Kuna watu ambao wamekuwa wakiiba vikingi vya stima na tunashangazwa na ni vipi tutawahudumia wananchi ilhali wengine wao wanajishughulisha na wizi wa vikingi," alishangazwa Machuka. 

Machuka aidha aliwasihi wananchi kujitokeza nakuripoti watu wanaowashuku kuhusika na wizi huo, huku akihimiza maafisa wa polisi kushirikiana na kampuni hiyo ili kuwanasa wahalifu. 

"Ni himizo langu kwa wananchi kujitokeza na kuripoti watu wanaowashuku kuhusika na wizi wa vikingi vya stima, na pia twaomba maafisa wa polisi kushirikiana nasi kwa kuwatia mbaroni washukiwa," aliongezea Machuka. 

Haya yanajiri baada ya kampuni hiyo kuanzisha mikakati ya kufidia familia ambayo nyumba yao iliangukiwa na vikingi vya stima kule Enchoro kaunti ya Nyamira hivi maajuzi.