Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwanasiasa kutoka eneo bunge la Likoni Hamisi Ali Moko, ambaye tayari ametangaza kuwania kitu cha ubunge cha eneo hilo amebainisha nia yake ya kuwashirikisha vijana wa mtaa maarufu kama mateja katika ratiba ya kazi za kujisimamia ya kuzoa taka katika eneo bunge hilo.

Hamisi amesema kuwa vijana hao wamesahaulika na serikali ya kitaifa na ile ya kaunti, na akadokeza azimio lake la kutaka kuwajumuisha kwenye mpango wake ambao ameanzisha wa kuwapa kazi za kuzoa taka mitaani.

Mwanasiasa huyo, kwenye mahojiano siku ya Jumamosi na mwandishi huyu katika eneo la Likoni ambapo alikuwa akishiriki kwenye mchango wa kuchangia kanisa moja alisema kuwa tayari amewatambua vijana hao na yupo tayari kuwapa nafasi zaidi iwapo atapewa mkono na wapiga kura wa eneo hilo.

“Hawa vijana mnaita mateja singependa kuwaita hivyo, hawa ni vijana kama wengine, ni wetu na sharti tuwape nafasi kwenye maisha ili kujiendeleza ndio sababu nimeonelea kuwaweka kimakundi ili tujiandae kuwapa kazi za kujisimamia,” alisema Hamisi.

Aliweka wazi kuwa kiongozi mzuri sharti awafikie watu anaowaongoza na si kukaa mbali na raia baada ya kuchukua madaraka jinsi ilivyo kwa viongozi wengi.