Wakazi katika Kaunti ya Mombasa wametakiwa kusaidia kuhubiri umoja na utangamano na kujiepusha na wanasiasa pamoja na viongozi wanaokuwa na lengo baya la kutaka kuwatawanya wakenya kwa misingi ya kikabila.
Kwa kuchukua hatua kama hizo za kuwahepa wanasiasa na viongozi wa kutoa matamshi ya uchochezi itasaidia kupunguza visa vya wakenya kubaguana haswa katika maeneo ya kazi pamoja na makazi ili kuimarisha uwepo wa mshikamano miongoni mwa wa wakenya na jamii mbali mbali zinazoishi nchini.
Akiongea jijini Mombasa na wanahabari siku ya Jumatatu, mkurugenzi mkuu wa tume ya uwiano na utangamano Hassan Mohamed alisema kuwa wananchi sharti wawe katika mstari wa mbele kuona kuwa wanaendeleza maono ya nchi, pamoja na kuwakanya vijana ambao mara nyingi ndio wanatumiwa na viongozi kugawa umma kwa misingi ya dini, rangi pamoja na ukabila.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa tume yake iko katika mstari wa mbele kuona kuwa viongozi wanaopatikana na au kushukiwa kutoa matamshi yanayowatenganisha na kuwachochea wakenya wanatiwa mbaroni na kukabiliwa kwa mujibu wa sheria.
Aidha, alitoa wito kwa viongozi kukoma kuwatumia vijana kwa maslahi yao ya binafsi, na badala ya kujihusisha katika harakati za kuwatawanya wakenya, ni vyema zaidi kuwaongoza wananchi kwenye miradi ya maendelea ili kuinua nchi.