Share news tips with us here at Hivisasa

Mahakama moja ya Nakuru imeagiza mwanamume mmoja anayekabiliwa na shtaka la ubakaji kufanyiwa uchunguzi kubaini iwapo ana matatizo ya kiakili.

Hii ni baada ya mshtakiwa kufikishwa mahakamani siku ya Jumatatu na kukiri shtaka la kumbaka mtoto wa miaka mitano kwa kiwango fulani huku pia akipinga shtaka hilo kwa kiwango fulani, jambo ambalo liliwapelekea waliokuwa mahakamani kusalia vinywa wazi.

Upande wa mashtaka ulidai kwamba mshtakiwa huyo, Benjamin Wanjohi, alimbaka mtoto huyo wa kike katika sehemu ya Matundu Ndundori, Kaunti ya Nakuru mnamo Septemba 2, 2015.

Hakimu Mkuu Liz Gicheha wa mahakama ya Nakuru aliagiza kesi hiyo iahirishwe hadi tarehe Novemba 23, 2015.

Hakimu mkuu huyo aidha aliagiza mshtakiwa afikishwe katika Hospitali Kuu ya Mkoa iliyoko mjini Nakuru kufanyiwa uchunguzi wa kiakili kubaini iwapo ana matatizo yoyote na iwapo anaweza kujibu shtaka hilo.

Ripoti hiyo ya daktari sasa inatarajiwa kuwasilishwa mahakamani kesi hiyo itakapoendelea Novemba.