Mtahiniwa mmoja wa Shule ya msingi ya Tonga Omonuri, wilayani Nyamira, alitoweka shuleni huku mtihani mkuu wa darasa la nane uking’oa nanga siku ya Jumanne.
Kulingana na Bundi Mochibi, babake mtahiniwa huyo kwa jina Edward Mochibi, mwalimu mkuu wa shule hiyo alifika nyumbani kwao siku ya Jumatatu na kuwaarifu kuwa mtoto wao alitoweka shuleni siku ya Jumapili.
Mwalimu huyo alisema kuwa walimtafuta kijana huyo bila mafanikio, na kuamua kwenda kubaini iwapo alikuwa ametorokea nyumbani kwao.
“Nilipigwa na butwaa mwalimu alipofika nyumbani na kunijulisha habari hiyo. Sijui la kufanya kwa sababu sina habari mtoto wangu aliko. Nilikuwa nafikiria yuko shuleni akijitayarisha kufanya mtihani,” alisema Mochibi.
Mochibi alisema kuwa baada ya kupokea ripoti ya kutoweka kwa mtoto wake, aliwapigia simu jamaa na marafiki lakini bado hajafanikiwa kumpata mtoto wake.
“Ninahofia kuwa mtoto wangu huenda asifanye mtihani huo iwapo hatapatikana,” alisema Mochibi.
Aliongeza: “Nawaomba wasamaria kunisaidia kumtafuta mtoto wangu.”