Kijana mwenye umri wa miaka tisa ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya msingi ya Kimuuni alikufa maji alipokuwa akivua samaki katika mto Mwitasyano, eneo la Ikombe, kaunti ndogo ya yatta.
Akidhibitisha kisa hicho siku ya Alhamisi, chifu wa Ikombe, Bwana Onesmus Nzile, alisema kuwa mtoto huyo alikuwa ameandamana na wenzake kwenda kuvua samaki katika mto huo alipoteleza na kuanguka mtoni.
"Mtoto huyo alikuwa ameenda na wenzake kuvua samaki katika Mto Mwitasyano pale alipoteleza na kufa maji kwani hakukuwa na mtu ambaye angeweza kumwokoa,” alisema Nzile.
Aliongeza, "Wazazi wanafaa kuwachunga watoto wao msimu huu wa mvua hasa ikizingatiwa kuwa shule zakaribia kufungwa ili kuwaepusha na majanga ya aina hii.”
Chifu huyo vilevile aliwaonya wazazi kuwa waangalifu na kutowaruhusu watoto kwenda mtoni peke yao kwani mito mingi imefurika na ni hatari kwa watoto.
Maiti ya mtoto huyo ilichukuliwa na maafisa wa polisi na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Matuu.