Mwakilishi wa eneo wadi ya Bokeira Karen Atuya amejitokeza kuwahimiza kina mama kuwania nyadhifa mbalimbali za kisiasa nchini.
Akihutubia wakazi wa eneo lake la uwakilishi kule Orwaki siku ya Jumanne, Atuya alisema kuwa yapaswa kina mama wajitokeze kuwania nyadhifa za kisiasa ili kubadilisha hali ya uongozi nchini.
"Tangu enzi kina mama wamekuwa wakidhalilishwa kwamba hawawezi wakawa viongozi, lakini ni himizo langu kwenu kina mama kujitokeza kuwania nyadhifa mbalimbali za kisiasa kwa maana nina hakika kwamba mtabadilisha hali ya uongozi nchini," alisema Atuya.
Atuya aidha aliongeza kwa kuwahimiza wakazi wa kaunti ya Nyamira kuwachagua viongozi wa kisiasa kwa misingi ya utendakazi wao na wala sio kwa kuzingatia vyama vya kisiasa.
"Tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao na ningependa kuwahimiza wapiga kura kuhakikisha kuwa wanawachagua viongozi wa kisiasa kwa kuzingatia utendakazi wao na walio sio vyama vya kisiasa wanavyoegemea," aliongezea Atuya.