Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwanabloga Waime Mburu anayekabiliwa na madai ya kumharibia jina Gavana wa Kiambu William Kabogo ameachiliwa huru na mahakama ya Mombasa.

Mwanabloga huyo anadaiwa kuandika taarifa mnamo Januari 8, 2016, iliyomhusisha Kabogo na biashara ya mayai yenye bei ya chini, hali aliyoitaja kukandamiza na kuharibu biashara ya uuzaji mayai nchini.

Aidha, anakabiliwa na mashtaka matatu huku jengine likiwa ni la kutumia vyombo vya mawasiliano vibaya.

Akitoa uamuzi wa kumuachilia mwanabloga huyo, Hakimu katika mahakama ya Mombasa, Nicholas Njagi, alisema kuwa ameondolea mwanabloga huyo mashtaka chini ya kifungu cha 87 cha katiba.

Hatua hii inhajiri baada ya afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma Alexendra Muteti, kuagiza kuondolewa mashtaka na kuachiliwa huru kwa mwanabloga huyo, baada ya polisi kukosa kuwasilisha ushahidi wa kutosha wa kumfungulia mashtaka dhidi yake.

Muteti aliambia mahakama kuwa aliagizwa na mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma nchini Keriako Tobiko kumuondolea mashtaka na kumuachilia huru mwanabloga huyo.

Hii ni baada ya wakili wa mwanabloga huyo, Adalla Boaz, kuwasilisha ombi mahakamani siku ya Ijumaa, kutaka mteja wake kuondolewa mashtaka hayo kwa kile alichokitaja kuwa ukandamizaji wa uhuru wa wanahabari.