Mwanamume wa umri wa makamo, kutoka eneo la Mkanganyi amehukumiwa kifo baada ya kupatikana na makosa ya kutekeleza wizi wa mabavu na mauaji.
Mnamo Aprili 16, 2011, mshukiwa Juma Kadenge akiwa amejihami kwa panga anadaiwa kuiba simu aina ya Nokia iliyo na thamani ya shilingi elfu kumi.
Aidha, baada ya kutekeleza wizi huo wa mabavu, mshukiwa anadaiwa kumkatakata Marehemu Halima kwa panga hadi kufariki.
Akitoa hukumu Ijumaa, hakimu Richard Odenyo alisema kuwa ushahidi uliotolewa unaonyesha kuwa mshukiwa alihusika katika wizi na mauaji hayo.
Odenyo alisema kuwa hukumu ya kifo itakuwa funzo kwake na kwa wengine wanaojihusisha na visa kama hivyo. Mshukiwa yuko na siku kumi na nne za kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.
Wakati huo huo, mahakama imemfunga miaka nne Dena Nzombo kwa kosa la kupatikana na simu ya marehemu Halima Muhidhin.