Share news tips with us here at Hivisasa

Mwili wa mwanamume ulipatikana ukiwa umetupwa kwenye mtaro katika eneo la Kabazi, Kaunti ya Nakuru.

Akidhibitisha kisa hicho, Afisa wa polisi katika eneo la Kirengero, Inspekta John Kimathi, alisema kuwa mwili wa marehemu, Samwel Ndungu, mwenye umri wa miaka 38, ulikuwa na damu puani na huenda alifariki katika hali ya utatanishi, kwa vile mshipi wake ulikuwa kando japo alikuwa na mavazi mengine.

Hata hivyo, Kimathi alisema kuwa daktari tu ndiye anaweza kudhibitisha kiini cha kifo cha marehemu, baada ya kufanya upasuaji.

Kulingana na wakazi ambao walizungumza na mwandishi huyu, wakiongozwa na Mzee Gitiba, marehemu alipatikana akiwa ametupwa kwenye mtaro siku ya Ijumaa.

Gitiba alisema kuwa wakazi waliita askari wa AP katika eneo hilo, ambao walifahamisha polisi wenzao kutoka Kirengero.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti mjini Nakuru.

Wakazi hao wamewataka polisi kuzidisha doria za usiku katika eneo hilo, ili kuzuia uhalifu ambao walisema umeanza kuchipuka upya