Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Maskuota 97 wa shamba la ekari 2,500 lililoko eneo la Kapsetek katika eneo la Rongai, Kaunti ya Nakuru wametishia kufanya maandamano wakisema msimamizi wa shamba hilo Maura Batla anakiuka haki zao.

Wakizungumza Alhamisi kupitia John Abok, wakazi walisema kwamba katika mwaka wa 1979, mmiliki wa shamba hilo Michael Batler, ambaye kwa sasa ni marehemu, alimpa kila skwota ekari mbili na nusu za shamba.

Waliongeza kuwa msimamizi wa shamba hilo kwa sasa Maura Batla amewafukuza kwenye vipande hivyo vya ardhi na kuwapa ekari 49 zilizoko mahala palipo na maporomoko ya udongo.

Wakionekana kugadhabishwa na swala hilo, wakazi hao walisema kuwa ni jambo la kuhuzunisha kwani wanaweza kukumbwa na mafuriko kutokana na mvua ambayo inashuhudiwa.

Batla alitangaza kuwa anawatambua maskwota 37 pekee na wengine 60 wanaopaswa kuondoka kwenye shamba lake haraka iwezekanavyo.

“Hatuwezi kuondoka kwa sababu hata makaburi ya mababu zetu yamo kwenye shamba hili,” alisema mmoja wa maskuota hao, John Arap Sang alisema.

“Ekari 49 za shamba haziwezi kututosha kutokana na idadi kubwa ya maskuota tuliopo hapa,” aliongeza Sang.

Mkazi mwingine, Margaret Elaman alidokeza kwamba wameenda kwa viongozi wa neo hilo la Rongai na hawajapata usaidizi wowote.

“Mmiliki wa shamba hili alifariki miaka 40 iliyopita na nawatambua maskuota 37 pekee, na hao wengine sijali watakapo kwenda hata dakika moja,” alisema Maura Batla, alipokua anazungumza na huyu mwandishi.