Viongozi wa Kaunti ya Nakuru wameitaka Tume ya uwiano na utangamano wa kitaifa NCIC kufanya mikutano ya amani inayoshirikisha vijana kote nchini.
Viongozi hao walisema hatua hiyo ni muhimu kwani kwani kundi hilo ndilo hupotoshwa zaidi wakati wa kampeni za uchaguzi.
Naibu Gavana wa Nakuru Joseph Ruto alisema vijana wanapaswa kujiepusha na kutumiwa na wanasiasa wenye maslahi ya kibinafsi kama vikaragosi, katika kile ambacho hakina manufaa kwa jamii pana ya Kenya.
Ruto alisema kwamba NCIC kupitia majukumu yake ya kuhakikisha usawa wa nafasi, mshikamano wenye amani, uwiano, na uadilifu, yafaa kusisitizia vijana umuhimu wa kukaa kwa amani na kujiepusha na maswala ya uchochezi ikiwemo siasa kali ambazo alisema ni tishio jipya kwa usalama wa Kenya.
“Najua kwamba vijana barubaru ndio huadhirika na siasa za kupotosha, na ndio pia hulengwa katika kushiriki ghasia. Hata hivyo, hayo yanaweza kubadilika ikiwa tutagundua kwamba jukumu la vijana katika jamii yetu ni kuweka msingi mzuri wa kijamii siku za usoni” aliema Ruto.
Akizungumza siku ya Jumanne kwenye warsha ya NCIC kuhusu amani, uwiano wa kitaifa na uadilifu, Ruto pia aliwapa changamoto vijana kutumia katiba na vifaa vingine vya kisheria kufanya maamuzi ambayo yatasongesha Kenya mbele.
“Nyinyi ndio viongozi wa sasa na wa kesho, na hiyo inawapa nguvu zaidi ya kuboresha Kenya,” alisema Ruto.
Aliongeza kuwa vijana ndio kundi kubwa na lenye uwezo mwingi nchini, na wanahitaji kuhusishwa katika mipango yote ya maendeleo.
Warsha hiyo ya siku mbili imeleta pamoja vijana kutoka kaunti za Nakuru na Kisii.
Mkurugenzi mkuu wa NCIC Mohammed Hassan alipongeza kaunti ya Nakuru ambayo imeorodheshwa ya 17 kati ya zote 47 katika kuzingatia maswala ya usawa na ugavi wa haki wa raslimali.
Hassan alisema hali hiyo imeleta uwiano na utangamano katika kaunti hiyo ambayo huwa ni makao ya jamii zote za Kenya.