Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wanahabari mjini Nakuru wametakiwa kusimamia haki na kuripoti ukweli na maovu yanayotendewa watu katika jamii wanapofanya kazi yao.

Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri amewataka wanahabari kutoegemea upande wowote wa kisiasa wanapoandika ripoti zako.

Ngunjiri amesema kuwa wanahabari hawafai kupendelea upande wowote wa kisiasa na kuwataka kutoshawishiwa kwa pesa.

"Watu wa habari mnafaa kutusaidia kueleza ukweli na kupigania haki ya watu wanaonyanyaswa katika jamii," alisema Ngunjiri.

Akiongea katika mkao na wanahabari jumapili katika hoteli moja hapa Nakuru, Ngunjiri alisema kuwa jamii itapotoshwa iwapo wanahabari watakuwa  watu wa kushawishiwa.

"Vyombo vya habari na wanahabari ni watu wa maana sana katika jamii na kwa hivyo mnatakiwa kuwa huru  kwa kuwa mkipendelea upande mmoja basi jamii haitapata haki," alisema.

"Nyinyi mnapaswa kutafuta habari kutoka pande zote wala msipendelee upande mmoja na muache  kuuandika habari zisizo sahihi, na muandike kuhusu watu wanaotumia mamalaka yao kuwanyanyasa wengine, " alisema.

Aidha, Ngunjiri alimshtumu spika wa bunge la kaunti ya Nakuru Susan Kihika kwa kile alichokitaja kama kuwaleta watu waliolipwa katika mikutano  ili wawapigie wapinzani wake kelele.

"Hii siasa ya kuwalipa watu na kuwanunulia pombe ili wapige makelele katika mikutano inafaa kukoma  na spika anapaswa kuwachana na hiyo siasa  chafu,"alisema.

Ngunjiri aliapa kuendelea kupiganaia haki za wanyonge katika eneo bunge lake na kumsuta spika wa bunge la kaunti ya Nakuru Susan Kihika kwa kuwatorosha wawekezaji kutoka eneo hilo.