Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Nakuru  Magharibi Samuel Arama amesema hajakihama chama cha Orange Democratic Movement (ODM) na kuingia kwenye muungano wa Jubilee.

Arama amesisitiza  yungali ndani ya ODM lakini akasema atazidi kushirikiana na serikali ya Jubilee ili kufanikisha maendeleo.

Akizungumza hii leo katika eneo la London, Mbunge huyo amesema kuwa chama si muhimu kwani kile kinachohitajika ni maendeleo.

"Chama ni chombo,  cha msingi ni utendkazi na kuwajibika, maswala ya maendeleo ndiyo kila Mkenya anahitaji wala si misingi ya chama," alisema Arama.

Aidha, Arama amesema ifikapo mwaka 2017 ataamua chama atakachotumia kuwania kiti hicho cha ubunge.

Katibu wa kaunti ya Nakuru Joseph Motari, ambaye aliandamana na Arama alisema viongozi wanafaa kujihusisha na maendeleo na wala si siasa za vyama.

"Maendeleo ni maswala muhimu kwa mwananchi na ninawapa changamoto wabunge wengine toka kaunti ya Nakuru ambao hawajakumbatia maendeleo katika eneo bunge lao," alisema Motari

"Nakuru Magharibi imekuwa sehemu iliyotengwa kwa muda lakini kwa sasa wakaazi wanaweza kuona tofauti kadha wa kadha," Motari aliongeza.