Huku shughuli ya kuwasajili wapiga kura ikiendelea humu nchini,vijana na wananchi kwa jumla wametakiwa kujiepusha na vurugu zozote katika vituo vya usajili.
Katika kikao na wanahabari Jumatatu, OCPD wa Nakuru Musa Kongoli alisema kuwa idara ya polisi itamchukulia hatua kali yeyote atakayejaribu kuleta vurugu katika shughuli hiyo.
Huku akisisitiza kwamba polisi wana wajibu wa kuhakikisha utulivu, pia aliwataka vijana kutohitilafiana na haki zao.
"Ningependa kutoa wito kwa vijana na wananchi Nakuru kwa jumla kuhakikisha kwamba wanadumisha amani,"Kongoli alisema.
Wakati huo huo, afisa mkuu huyo wa polisi Nakuru alivitaka vyombo vya habari kuwa mstari wa mbele kuhubiri amani.
"Nyinyi wanahabari pia mna wajibu mkubwa wa kuhubiri amani na nawasihi mtusaidie,"akaongeza Kongoli. Vilevile ametoa wito kwa wakaazi wa Nakuru kushirikiana na polisi kumaliza uhalifu.