Magavana wa kaunti za Kisii na Nyamira wamelahumiwa vikali kwa kutohudhuria mkutano wa kuwaleta pamoja ili kuzungumzia mzozo unaoendelea kushuhudiwa katika soko la Keroka.
Hii ni baada ya mkutano kupangwa katika mji wa Keroka mnamo siku ya Alhamisi ili kuwaleta pamoja magavana James Ongwae wa Kisii na John Nyagarama wa Nyamira ili kuamua ni wapi mpaka wa kutenganisha kaunti hizo mbili ulipo mjini Keroka.
Wakizungumza siku ya Alhamisi mjini Keroka wazee wa jamii ya Kisii wakiongozwa na Joseph Moreka walisema viongozi hao ndio huchangia ghasia kushuhudiwa katika soko hilo la Keroka kila wakati maana wamekataa kujiunga pamoja kutafuta suluhu.
“Jinsi tumeona viongozi hawa ndio hutufanya sisi wananchi kugombana wenyewe kwa wenyewe maana tuliwaalika hapa Keroka na hakuna yeyote aliyekuja ata kusema kile kilimfanya kutohudhuria mkutano,” alisema Moreka.
“Tunaomba viongozi hao kutuambia ni wapi mpaka wa Keroka unapitia ili kupunguza mizozo kushuhudiwa kila wakati,” aliongeza Moreka
Juhudi zetu za kuwatafuta viongozi hao ziligonga mwamba huku waziri wa ardhi katika kaunti ya Nyamira Richard Mareri akisema kuwa hakuna mzozo mpakani Keroka na kusema mambo hayo yalizungumziwa hapo awali na suluhisho lilipatikana.