Tume ya kudhibiti kawi nchini ERC imesema itatoa orodha ya vituo vya mafuta ambavyo vimekuwa vikiwauzia Wakenya mafuta ya petroli yaliyochanganywa na yale ya taa.
Akizungumza siku ya Jumatano kwenye kikao na wanahabari katika ufunguzi wa warsha ya kuwahamasisha walio katika sekta za mafuta na umeme, Mkurugenzi mkuu wa Tume ya ERC mhandisi Joe Ng’an’ga alisema orodha hiyo huenda ikatolewa katika muda wa wiki moja ijayo, na itachapishwa kwenye magazeti makuu ya Kenya.
Kwa muujibu wake, orodha hiyo itakuwa na maelezo kuhusiana na vituo vyote vilivyofungwa, lini vituo hivyo vya mafuta vilipatikana na kosa hilo na hatua iliyochukuliwa dhidi ya vituo hivyo.
Ng'ang'a alisema kwamba mojawapo ya adhabu ambazo zitatolewa kwa wanaopatikana na makosa hayo ni kuadhibiwa vikali kama vile kutozwa faini ya shilingi milioni moja baada ya kufikishwa mahakamani.
Hata hivyo, alisisitiza kukomeshwa kwa kosa hilo na kutaka mashirika mbalimbali, taasisi za serikali za kaunti, taasisi za serikali za kitaifa na wadau mbalimbali hapa nchini kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa tabia hiyo inatokomezwa.
Warsha hiyo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali kama vile wawakilishi kutoka kwa Wizara ya Kawi, serikali za kaunti zilizo kwenye eneo la bonde la ufa, mamalaka ya ukusanyaji wa ushuru (KRA), kampuni ya mafuta ya Kenya Pipeline na Taasisi ya Teknolojia ya RVIST miongoni mwa wadau wengine.