Kamati ya uhasibu na uwekezaji wa pesa za umma kwenye bunge la Kaunti ya Nyamira PIAC imeanzisha uchunguzi kuhusiana na utoaji zabuni unao wahusisha maafisa wakuu wa kaunti hiyo.
Kulingana na mwenyekiti wa kamati hiyo Ezra Mochiemo, muungano wa vijana kwenye kaunti hiyo almaarufu ‘Youth Senate’, ulikuwa umeiandikia barua ya kuitaka kamati hiyo kuishinikiza serikali ya kaunti hiyo kuchapisha majina ya wanakandarasi wote hasa kina mama, vijana na watu wanaoishi na ulemavu waliopewa kandarasi tangu mwaka wa 2013.
"Nilipokea barua hiyo kutoka kwa spika wa bunge hili Joash Nyamoko na tayari tumeanzisha uchunguzi ikiwa kweli vijana, kina mama na watu wanaoishi na ulemavu wamekuwa wakipokezwa asilimia 30 ya kandarasi hizo. Tunataka kuishinikiza serikali ya kaunti hii kuchapisha majina yote ya wanakandarasi walionufaika na kandarasi hizo tangu mwaka wa 2013," alisema Mochiemo.
Mochiemo aidha alisema kuwa kamati yake itazipa pande zote mbili nafasi za kuwasilisha ripoti mbele ya kamati hiyo, ili uchunguzi ufanywe kuhusiana na madai ya mapendeleo kwenye utoaji wa kandarasi katika kaunti ya Nyamira, kisha ripoti kuwekwa wazi chini ya mwezi mmoja.
"Hili ni suala lililo na uzito mkubwa sana na kamati yangu itazipa pande zote mbili nafasi ya kuwasilisha tetezi zao. Tunahitaji kujua ukweli kuhusiana na suala hili, ili nasi tufanye uchunguzi wetu na kisha kuweka bayana ripoti kuhusiana na suala hili chini ya mwezi mmoja ujao," aliongezea Mochiemo.