Share news tips with us here at Hivisasa

Uhusiano mwema na ushirikiano baina ya maafisa wa polisi na vijana katika Kaunti ya Mombasa umetajwa kama njia mojawapo ya kupunguza visa vya uhalifu katika maeneo mbalimbali.

Afisa kutoka shirika lisilo la kiserikali la Kenya Community Support Centre (KECOSCE) Mwalimu Rama amesema kuwa bila ya ushirikiano mwema baina ya vijana na idara ya polisi, kudorora kwa usalama katika Kaunti ya Mombasa kutaendelea kuwa donda sugu.

Akizungumza katika kikao siku ya Jumatano kilicholeta pamoja maafisa kutoka mashirika mbalimbali ya kijamii, vijana, sawia na maafisa wa polisi katika eneo bunge la Changamwe, Rama alisisitiza kuwa kuna haja ya kitengo cha polisi kubadilisha nadharia waliyo nayo kuwachukulia kila kijana kama mshukiwa wa uhalifu.

Aliwataka maafisa wa polisi kudumisha uhusiano mwema baina yao na vijana ili kufanikisha jukumu la kuimarisha usalama.

Aidha, alidokeza kuwa idadi kubwa ya vijana wameshindwa kutoa taarifa muhimu kwa idara ya polisi kwa kile walichokitaja kama kuhangaishwa na kunyanyaswa na maafisa wa polisi.

“Vijana wengi wamepoteza matumaini na idara ya polisi kutokana na mbinu wanazochukua, huku wengine wakiwakemea kwa kutumia nguvu kupita kiasi,” alisema Rama.

Aliongeza, “Ni kutokana na visa kama hivi ambavyo vimepelekea vijana kupoteza matumaini na idara ya polisi wakidai kunyanyaswa.”

Rama alisema ufanisi na utulivu katika miji tofauti katika Kaunti ya Mombasa inapatikana iwapo uhusiano mwema na uwiano utakuepo baina ya idara ya polisi na vijana.

Wakati huo huo afisa wa oparesheni kutoka kituo cha polisi cha Changamwe Geofrey Walumbe ametoa onyo kwa maafisa wa polisi wenye desturi ya kuwanyanyasa vijana na Wakenya kwa jumla.

Alisema kuwa watachukuliwa hatua za kisheria kwa kile alichokitaja kama kwenda kinyume na maadili ya huduma kwa wananchi.

Vilevile afisa huyo amebaini kuwa visa vya uhalifu na utumizi wa mihadarati katika maeneo ya Changamwe vimepungua maradufu kutokana na ushirikiano baina ya wakazi na polisi.