Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Idara ya usalama katika Kaunti ya Mombasa imetakiwa kuwa kipaumbele katika kutoa ulinzi wa kutosha kwa waendeshaji badaboda.

Haya yanajiri baada ya kushuhudiwa visa vya mauwaji ya waendeshaji bodaboda hao.

Kauli hii ilitolewa na mwenyekiti wa muungano wa waendeshaji bodaboda katika eneo la Likoni Salim Mangale, ambaye alisema kuwa usalama kwa wahudumu wa bodaboda umekuwa dhaifu ikizingatiwa wanavamiwa kila uchao.

Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu, baada ya kumzika mmoja wao ambaye aliuwawa kwa kukatwa katwa kwa panga na watu wasiojulikana wiki iliyopita, Mangale aliwataka waendeshaji bodaboda kushirikiana katika kuwafichua wahalifu hao.

Mangale aliitaka idara ya usalama kuchunguza na kuwachukulia hatua za kisheria wahalifu wanaohusika katika visa hivyo vya mauwaji.

Aidha, aliongeza kuwa tangu mwezi Aprili mwaka jana, takriban waendeshaji bodaboda wanane wameuwawa kwa kukatwa kwa panga na kuaga dunia papo hapo, huku wengine wakikata roho wakiendelea kupokea matibabu hospitalini.