Maafisa wa polisi wilayani Manga, kaunti ya Nyamira wameanzisha uchunguzi dhidi ya kifo cha Evans Omwenga aliyepatikana ameaga dunia nje ya duka la jirani yake Jumatatu.
Mwanamume huyo anadaiwa kwenda kununua sigara kwa duka la jirani yake ambapo alipatikana ameaga dunia.
Akizungumza na waandishi wa habari, katika eneo la Motembe chifu wa lokesheni ya Kiamakondo Christus Makori alisema mwanamume huyo alipatikana ameaga dunia na chanzo cha kifo hicho hakijabainika wazi hadi sasa.
Kulingana na chifu huyo, maafisa wa polisi wilayani Manga wameanzisha uchunguzi ili kubaini jinsi mwanamume huyo aliaga dunia na hatua kali kuchukuliwa ikipatikana kuwa aliuliwa.
Makori alisema kuwa mwenye duka anadai kuwa marehemu alienda kununua sigara na baadaye wakashtukia marehemu ameaga nje ya duka lake.
“Kifo cha mwanamume huyu hakichabainika wazi lakini maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi ili kubaini jinsi marehemu aliaga,” alisema Christus Makori.
“Baada ya uchunguzi kufanywa na kukamilika ndiposa tutajulisha wananchi lakini kwa sasa hakuna anayeshukiwa kuhusika na kifo cha mwanamume huyu lakini uchunguzi unaendelea,” aliongeza chifu Makori.
Katika siku za hivi maajuzi,visa vya watu kupatikana wameaga na wengine kuawa katika kaunti ya Nyamira vimekuwa vikiongezeka huku kamishena wa kaunti hiyo Josephine Onunga akiombwa kuimarisha usalama.