Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwenyekiti wa matatu katika kituo cha Magari mjini Kisii, amewaomba maafisa wa polisi kuwatia mbaroni baadhi ya wafanyibiashara katika kituo hicho wanaojihusisha na ulanguzi wa dawa za kulevya.

Samson Mose alisema kuwa kuna baadhi ya wafanyibiashara katika kituo hicho wanaouza pombe haramu pamoja na mihadharati kwa kisingizio cha kufanya biashara tofauti.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne mjini Kisii, Mose alisema kuwa idadi kubwa ya wahudumu wa matatu ndio hutumia dawa hizo.

Aliwataka maafisa wa polisi kufanya msako na kuwatia mbaroni wafanyibiashara hao na kuwaondoa katika kituo hicho.

Kulikua na ripoti hapo awali kuwa baadhi ya wauza mboga katika kituo hicho wanajihusisha na biashara hiyo ya mihadarati na pombe haramu.

“Wahudumu wa matatu katika kituo cha magari mjini Kisii wanasifa mbaya kwa sababu wanatumia mihadharati na pombe haramu ambayo wanauziwa na wafanyibiashara hao,” alisema Mose.