Naibu Rais William Ruto amekosa kauli za wapinzani kwamba serikali ya Jubilee haijafanya mradi wowote kwa manufaa ya mwanchi.
Akizungumza huko Ganda, Kaunti ndogo ya Malindi wakati wa kampeni ya mgombea kiti cha eneo bunge la Malindi, Philip Charo siku ya Jumanne, Ruto alipuzilia mbali kauli hizo na kusema kuwa hizo ni porojo tu za upinzani.
Alisema kuwa Jubilee inajitahidi pakubwa katika kutekeleza maazimio yake ya maendeleo kwa taifa.
Naibu rais huyo alitaja mradi wa huduma kwa vijana wa taifa NYS na huduma za wanawake waja wazito kujifungua bila malipo kama baadhi ya miradi ya maendelao ambayo serikali imetekeleza.
Aidha, aliongeza kuwa Jubilee bado inajitahidi katika kutimiza miradi muhimu kwa wananchi wa taifa zima bila ubaguzi wowote.
Kauli yake inajiri baada ya baadhi ya viongozi wa mrengo pinzani wa Cord kudai kuwa Jubilee haitekelezi miradi yoyote yenye manufaa kwa jamii, na kudai kuwa inaendeleza utumizi mbaya wa rasilimali za umma na ufisadi nchini.