Huku uchanguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi ukikaribia, seriakali ya JAP imeahidi kuwa itatoa hati miliki za mashamba zaidi ya elfu 700 ili kuwaepusha wakazi wa maeneo ya Pwani kuhangaishwa na kufurushwa mara kwa mara na wengi wao kubakia maskwota.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika eneo la Malindi, kwenye harakati za mwisho za kumpigia debe mgombeaji wa JAP, Naibu Rais William Ruto alisema kuwa serikali iko tayari kuwafaidi wakazi wote bila kuzingatia mirengo na misimammo yao ya kisiasa wala walikopigia kura.
Ruto aliwahakikishia wakazi kuwa serikali haina nia yoyote ya kuwatenga bali lengo la serikali ya Jubilee ni kuwapatanisha Wakenya wote na kuona kila raia ana haki zake.
Aliwarai wenyeji kumpigia muwaniaji wa chama cha JAP Philip Charo kura ili wawe kwenye upande wa serikali.
Ruto aliwasuta viongozi wa upinzani kwa kuendelea kutumia porojo kwa kujaribu kupaka tope serikali na kusema kuwa mrengo wa Cord hauna lolote la kuwapa wakazi wa Pwani na kuwa wamejikita tu kwenye upigaji siasa bila vitendo.
“Serikali kwa miaka mitatu imetoa zaidi ya hati miliki za mashamba elfu 300 na sasa serikali ina mpango wa kutoa zaidi ya hatimiliki elfu 700 kwa wakazi,” alisema Ruto.