Naibu gavana wa Kaunti ya Nakuru amesema kuwa wakazi pamoja na Wakenya kwa jumla watajilaumu wenyewe kwa kuwachagua viongozi wasiyo na maadili na ambao hawawajibikii majukumu yao.
Joseph Ruto alisema kuwa viongozi hao watajipata katika uongozi ikiwa wananchi hawatawajibika kidemokrasia kwa kupiga kura ili kuwaondoa viongozi hao.
Akizungumza siku ya Jumamosi wakati wa sherehe za maadhimisho ya siku ya Jamhuru katika uwanja wa Afraha, Mjini Nakuru, Ruto aliwataka vijana waliyohitimu umri wa miaka 18 kujiandikisha ili waweze kujipatia vitambulisho vya kitaifa.
Alisema kwamba baada ya kujipatia vitambulisho hivyo vya kitaifa, vijana wanapaswa kujitokeza na kujiandikisha katika tume ya IEBC, wakati zoezi hilo litakapo zinduliwa kwa ajili ya matayarisho ya zoezi la kupiga kura la mwaka wa 2017.
Naibu gavana huyo alisema kuwa asilimia kubwa ya idadi ya watu humu nchini ni ya vijana hivyo basi iwapo watashikana kwa pamoja na kupata muongozo na kufanya uamuzi ufaao, bila shaka watakuwa na viongozi bora.
Matamshi haya ya kiongozi huyo yanajiri baada ya mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini, IEBC, Isaac Hassan, kutangaza kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017 utafanyika Agosti 8, 2017.