Seneta wa Kaunti ya Nyamira Kennedy Okong'o ameshtumu vikali hatua ya walimu wakuu wa shule za umma kuongeza karo bila yakuwashirikisha washikadau.
Akihutubu kule Chepilat siku ya Jumatatu, Okong'o alisema walimu wakuu wa shule nyingi wamekuwa wakiongeza karo kisiri bila ya kuihusisha wizara ya elimu, hatua aliyosema serikali ya kitaifa inastahili kuichunguza na kuwachukulia hatua za kisheria walimu hao.
"Mimi naunga mkono masomo kwa watoto wetu ila kuna baadhi ya walimu ambao bado wanaongeza viwango vya karo kwa wazazi. Wakuu wa shule hizo huwafukuza wanafunzi wanaokosa kulipa fedha hizo na hali kama hii ndiyo tunayotaka kuona kuwa haishuhudiwi," alisema Okong'o.
Seneta Okong'o aidha aliwashtumu wakurugenzi wa elimu kwenye kaunti kwa kutowachukulia hatua za kinidhamu walimu kama hao.
Alisema kuwa serikali ya kitaifa inafaa kuwachunguza na kudadisi utendakazi wa wakurugenzi hao.
"Baadhi ya wakurugenzi wa elimu kwenye kaunti hawajakuwa wakifanya kazi yao kwa uwazi, na ndio maana ninaitaka serikali ya kitaifa kuchunguza utendakazi wa wakurugenzi hao," alisema Okong'o.