Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Serikali ya Kaunti ya Nyamira imeaanzisha mikakati yakumaliza ujenzi wa soko la Miruka ambao ulikuwa umesitishwa kwa mwaka wa tatu sasa.

Akihutubu siku ya Jumanne alipotembelea soko hilo, katibu katika kaunti ya Nyamira Erick Aori, alisema kuwa tayari afisi yake imewaagiza wanakandarasi kurejea kwenye soko hilo ili kumaliza ujenzi uliosimamishwa kutokana na kuwepo kwa tofauti kati ya wafanyibiashara na wanakandarasi wa eneo hilo.

"Kwa kweli kumekuwa na tofauti baina ya serikali na wafanyibiashara wa eneo hili lakini sasa wakati umefika kwa wanakandarasi waliositisha ujenzi huu kurejelea majukumu yao kwa haraka. Tunahitaji kuona kuwa ujenzi wa soko hili umekamilika kwa haraka ili shughuli za biashara zirejelewe mapema mwakani," alisema Aori.

Hata hivyo, katibu huyo alikwepa kugusia swala la iwapo wafanyibiashara katika eneo hilo watalipa kodi ambayo wamekuwa wakidinda kuilipa kwa mwezi mmoja sasa, kutokana na madai ya kutokuwepo kwa huduma muhimu katika soko hilo.

"Kwa sasa singependa kugusia suala la iwapo mtalipa kodi kwa serikali au la kwa kuwa la muhimu sasa ni kwa serikali kuhakikisha kuwa ujenzi wa soko hili umekamilika. Baada ya hapo tutapanga vile shughuli zitakavyo endeshwa kwenye soko hili," alisema Aori.

Wafanyibiashara katika eneo hilo walisema kuwa hatua ya serikali ya kaunti hiyo kumaliza ujenzi wa soko hilo utawezesha kutekeleza shughuli zao katika mazingira mazuri.