Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mshauri wa masuala ya kifedha katika Benki ya Dunia, tawi la Kenya, ameitaka serikali ya Kaunti ya Nyamira kuweka mikakati yakuhakikisha kuwa wadi zinapokezwa pesa zakutosha za kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akihutubia wakazi wa Gachuba siku ya Jumapili, Charles Mochama alisema kuwa iwapo serikali ya kaunti itazingatia hilo, basi wawakilishi wadi wataweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa urahisi.

Mochama alisema kuwa shillingi millioni tatu zinazopokezwa wadi zafaa kuongezwa hadi millioni 7 ili kufadhili miradi muhimu.

"Pesa za ustawi wa wadi ni muhimu sana katika enzi hii ya serikali za ugatuzi. Watu wengi wamekuwa wakiwalaumu wawakilishi wadi kwa kutotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo bila kujua kuwa shillingi millioni tatu wanazopokezwa haziwezi tosha kufadhili miradi muhimu. Serikali ya kaunti yafaa kuwapokeza wawakilishi wadi shillingi millioni saba ili miradi ya maendeleo mashinani kuafikiwa," alisema Mochama.

Mochama alisema kuwa hatua ya fedha hizo kuongezwa itasaidia pakubwa wananchi kutoilaumu serikali ya kaunti hiyo kwa kutozingatia maendeleo.

Alisema kuwa sharti kamati maalumu ziteuliwe ili kuchunguza pesa zitakazopokezwa maeneo wadi zitakavyo tumika.

"Ikiwa pesa za maendeleo zitasalia kwenye serikali za kaunti bila kufikia maeneo wadi, basi itakuwa vigumu kwa kaunti hii kustawi. Sharti kamati maalum ziteuliwe ili kuchunguza jinsi wawakilishi wadi watakavyo tumia pesa hizo,” alisema Mochama.