Share news tips with us here at Hivisasa

Sekta ya utalii katika eneo la Pwani huenda ikaimarika zaidi siku za hivi karibuni kufuatia mpango wa serikali unaolenga kupanua uwanja wa ndege wa Malindi ili kurahisisha usafiri ndani na nje ya eneo hilo kwa wageni.

Katika ziara yake mjini Malindi mwishoni mwa juma, Naibu Rais William Ruto alisema tayari serikali imetenga shilingi milioni mia tatu ili kufanikisha upanuzi wa uwanja huo kwa lengo la kuimarisha sekta ya utalii nchini.

‘’Tunajua ya kwamba hapa Pwani ni eneo ambalo hupokea wageni wengi wakiwemo wakigeni na wa humo nchini ivyo lazima tuimarishe idara ya usafiri ili wageni wetu wasipate ugumu wa kusafiri,’’ alisema Ruto.

Ruto vilevile alisema kuwa serikali imetenga fedha ambazo watafidiwa wakazi watakaoadhirika kutokana na ukarabati wa barabara ya Malindi-Mombasa hadi Lungalunga.

Naibu Rais aidha alisema upanuzi wa uwanja wa ndege wa Malindi unatarajiwa kuanza mapema mwezi huu wa Januari.

Kenya ilishuhudia ongezeko la idadi ya watalii mwaka uliopita ukilinganishwa na 2014, huku wadau wengi wa sekta hiyo wakitaja kuimarika kwa usalama nchini kama moja wapo ya mambo yaliyochangia hali hiyo.