Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kiongozi wa vijana katika eneo la Kisauni amesema kuwa huenda idara ya usalama katika Kaunti ya Mombasa ikapatwa na changamoto za kukabiliana na magenge ya kihalifu iwapo swala la usalama litakosa kuangaziwa haraka iwezekanavyo, baada ya kufariki kwa afisa mkuu wa polisi kisiwani Mombasa Martin Asin.

Kulingana na Maxwell Masai, juhudi za afisa huyo mkuu wa polisi kisiwani Mombasa za kukabiliana na wahalifu zilikuwa zimefikia kiwango cha kusitisha uhalifu mjini humo.

Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatano, Masai alisema kuwa kuna haja ya idara hiyo kuteua afisa mwingine mkuu mara moja ili kuzuia kushuhudiwa kwa visa vya kihalifu vinavyotekelezwa na vijana mjini Mombasa.

“Kwanza tunasikitika kumpoteza afisa wetu mkuu wa polisi Mombasa lakini tunaiomba idara ya polisi kuchukua hatua za dharura kuteua afisa mwengine mkuu ili kuendeleza juhudi za Asin za kukabiliana na wahalifu kwa sababu bila ya kuwepo na usalama, basi eneo hilo litakuwa hatari zaidi,” alisema Masai.

Kiongozi huyo wa vijana alimtaja afisa huyo mkuu wa polisi kisiwani Mombasa kama afisa aliyejali mahitaji ya wakaazi, afisa muadilifu na kiongozi shupavu.

Masai aliwahimiza vijana kujitenga na uhalifu na kudumisha amani.