Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali za kaunti na ile ya kitaifa zimeombwa kutenga pesa ambazo zitatumika kugharamia matibabu ya wagonjwa wa saratani.

Haya yanajiri baada ya kubainika kuwa gharama ya kutibu ugonjwa huo ni ghali mno, huku wachache wakilazimika kusafiri nchini India kutafuta matibabu hayo, na wengine wakiishia kupoteza maisha yao kufuatia hali ya umaskini.

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatano mjini Kisii, wakaazi wa kaunti ya Kisii walisema huwa vigumu kupata matibabu ya saratani na kuomba serikali kutenga pesa ili kutoa usaidizi kwa waathiriwa wa ugonjwa huo.

“Tunaomba serikali yetu kujali maslahi ya wakaazi maskini ambao hawajiwezi. Tunaihimiza serikali kutenga pesa ambazo zitagharamia matibabu ya ugonjwa wa saratani humu nchini,” alisema Damaris Moikoba, mkaazi.

Aidha, wakaazi hao waliomba serikali kujaribu kila iwezalo kuandaa kambi za kupima ugonjwa wa saratani mara mbili kwa mwaka, ili wakaazi wengi waweze kupata fursa ya kupimwa na kujua hali zao za kiafya.

“Wakaazi maskini wanaougua ugonjwa wa saratani wanaendelea kuteseka na itakuwa vizuri iwapo serikali itaingilia kati na kuwasaidia wagonjwa hao kwa kukagharamia matibabu yao,” alisema Victor Gichana mkazi.