Serikali imetakiwa kutilia mkazo maswala ya kukuza talanta katika taasisi za elimu humu nchini, ili kuhakikisha wanafunzi wanaokamilisha masomo wana uwezo wa kujiendeleza maishani pasina kutegemea kuajiriwa.
Akizungumza siku ya Ijumaa kwenye mahojiano na mwandishi huyu katika eneo la Murunyu, Gerishon Kuria, mkurugenzi wa shule moja ya upili ya wasichana ya kibinafsi katika eneo la Murunyu, Lanet, alisema kuwa mfumo wa elimu uliopo humu nchini umetilia maanani ufanisi wa mitihani.
Kuria alisema kuwa hatua hiyo imelemaza maendeleo katika jamii kwa ukosefu wa ubunifu.
Mkurugenzi huo alisema kuwa mfumo wa sasa wa elimu huenda ukawaathiri baadhi ya wanafunzi hasa wale ambao maswala ya masomo darasani yanawapa changamoto.
“Kuna umuhimu wa kuwapa wanafunzi fursa ya kuchagua masomo ya darasani au hata talanta katika kujiendeleza maishani, pasina kusukumiwa masomo ambayo hayana manufaa kwa baadhi yao,” alisema Kuria.
Wakati huo huo, alipongeza hatua ya serikali katika kupiga jeki maswala ya elimu humu nchini, hasa ikizingatiwa kwamba idadi ya wanafunzi wanaoendelea kupata elimu kupitia mfumo wa elimu bila malipo katika shule za umma inazidi kuongezeka kila mwaka.
Hata hivyo, Kuria alitoa wito kwa serikali kushirikiana na sekta za kibinafsi katika kufanikisha sekta ya elimu humu nchini.