Share news tips with us here at Hivisasa

Mwakilishi wa wadi ya Bogichora Beautah Omanga ameiomba serikali ya kitaifa kuhakikisha kuwa maafisa wa utawala hasa machifu na manaibu, wamepokezw pikipiki kama njia mojawapo ya kuimarisha usalama Nyamira.

Akihutubu kwenye hafla ya mazishi katika eneo la Ramba siku ya Jumatatu, Omanga alisema kuwa chifu wa eneo hilo huwa na ugumu wa kushirikiana na maafisa wa usalama, kwasababu ya ukosefu wa namna ya usafiri wa haraka.

"Iwapo serikali kwa kweli imejitolea kuimarisha usalama mashinani, sharti machifu wapokezwe pikipiki zitakazo wawezesha kusafiri kwa haraka ili kuthibiti visa vya uhalifu," alisema Omanga.

Omanga aidha aliwahimiza wakazi wa eneo hilo kushirikiana kiukamilifu na maafisa wa usalama ili kuimarisha usalama, huku akiishtumu serikali ya kitaifa kwa kutoweka mikakati ya kuwapokeza pikipiki machifu kote nchini.

"Ninawaomba wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama ili kuthibiti visa vya uhalifu, kwa kuwa udumishaji usalama hauwezi ukakabiliwa iwapo ushirikiano wa wananchi utakosekana. Ni jambo la kushangaza kuwa serikali kuu haijawapokeza machifu kote nchini pikipiki ili kuimarisha usalama," aliongezea Omanga.