Viongozi wa shirika lisilo la serikali la kutetea haki za binadamu Muslim for Human Rights (Muhuri) wameelezea furaha yao na kutaja uamuzi wa mahakama wa kuamuru kufunguliwa kwa akaunti zao kuwa wa haki na kusema kuwa wataendelea kufanya kazi yao bila kuhofia.
Viongozi hao ambao waliongea nje ya mahakama makuu ya Mombasa siku ya Alhamisi baada ya uamuzi huo, walisisitiza kuwa hawakuwa na hatia na kazi yao ni kutetea haki za wanyonge na wale wasiokuwa na nafasi ya kujitetea katika idara za sheria katika nchi.
Bi Topster Juma, mmoja wa afisa wa shirika hilo alieleza kuwa sasa wanaweza kufanya kazi yao bila vikwazo ikizingatiwa kazi yao ya kuwasilisha malalamiko ya wateja wao mbele ya majukwaa ya kisheria inahitaji pesa ili shughuli ziweze kutekelezeka.
Shirika hilo ambalo lina afisi zake kwenye Kaunti zote sita za eneo la Pwani, lilijipata kwenye zogo hilo la kufungwa kwa akunti zao mapema mwaka huu kwa madai kuwa baadhi ya mashirika nchini yalikuwa yanaunga mkono vitendo vya uhalifu kama vile ugaidi, hali ambayo ilisukuma serikali kukwamiza harakati za mashirika hayo likiwemo Muhuri.
Uamuzi huo ulifaidi pia shirika la Haki Africa, ambalo nalo lilifungiwa akaunti zake za benki sawia na mashirika mengine.