Share news tips with us here at Hivisasa

Shughuli ya utoaji hati miliki kwa maskwota wanaoishi katika Shamba la Waitiki la zaidi ya hekari 900 katika eneo la Likoni, Kaunti ya Mombasa, itaanza siku ya Jumamosi.

Mbunge wa Likoni Masoud Mwahima amesema kuwa hatua hiyo imeafikiwa vyema na kamati inayosimamia shughuli hiyo ili kutoa nafasi kwa masorovea kukamilisha zoezi la kuweka mipaka.

Akizungumza na wanahabari katika eneo la Likoni mjini Mombasa siku ya Jumanne, Mwahima alisema kuwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye anataraijiwa kutoa hati miliki hizo kwa maskwota zaidi ya elfu 11 wanaoishi katika shamba hilo, anafahamu vyema shughuli hiyo na kuwataka wakazi kuwa na subra.

Aidha, amewataka wakazi kuwapuuza viongozi wa kisiasa wanaoeneza propaganda kuwa hati miliki hizo zinatolewa kama kigezo cha kuwachagua viongozi wa mrengo wa Jubilee katika uchaguzi mkuu ujao.

"Ningependa kuambia wakaazi walionichagua kuwa mpango huu sio wa kisiasa. Mpango huu unafanya kwa minajili ya kuwasaidia wakaazi wa Likoni kutofurushwa na mmiliki wa shamba hilo.,” alisema Mwahima.

Aliongeza, “Ningependa kuwaomba kuwa na subra kwani mutapewa hati miliki za shamba hili. Musikubali kudanganywa na watu kwa misingi ya kisiasa.”

Zaidi ya maskwota elfu nne wanaoishi katika shamba hilo la Waitiki wanatarajiwa kupata hati miliki hizo katika hafla itakayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.