Sekta ya utalii nchini na hususan eneo la pwani itaimarika hata zaidi baada ya kushuhudiwa kuwasili kwa meli ya kitalii katika bandari ya Mombasa mwaka huu wa 2016.
Hii ni baada ya kuwasili kwa meli ya watalii ya Ms Seven Seas Voyager yenye zaidi ya watalii 1000 katika Bandari ya Mombasa Jumamosi 2, asubuhi ikiwa meli ya tano kuwasili tangu mataifa ya Magharibi kuondoa marufuku ya raia wao kutozuru humu nchini.
Akiongea na wanahabari baada ya kupokea watalii hao katika Bandari ya Mombasa siku ya Jumamosi, waziri wa utalii nchini Najib Balala amesema kwamba sekta hiyo inatarajiwa kupata meli zengine zaidi mwaka huu.
“Tumepanga mikakati mwaka huu ya kuimarisha sekta ya utalii nchini na hususana eneo la Pwani na kuwasili kwa watlii zaidi ya elfu moja ni furaha kwetu kwa uchumi wa nchi utaimarika,” alieleza Balala.
Kwa upande wake meneja mkuu wa shughuli za Bandarini Mombasa Twalib Khamis amesema kwamba kwa ushirikiano na idara za usalama, wadau wa sekta ya utalii na wasimamizi wa Bandari hiyo, utalii unatarajiwa kuimarika zaidi na kukuza uchumi nchini.
Hata hivyo watalii hao wamezuru katika sehemu mbalimbali za kitalii ikiwemo kisiwani Mombasa, bunga za wanyamapori ya Mwaluganje, Shimba hills, Amboseli pamoja na maeneo mengine ya kitalii.