Daktari kutoka kituo cha Coast Hospice kule Mombasa amesema kuwa ugonjwa wa saratani unazidi kuongezeka katika eneo la Pwani.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne, Dkt Erick Amisi alisema kuwa kupuuza na ukosefu wa kusoma ndio sababu kuu za watu wengi kupoteza maisha yao kutokana na ugonjwa wa saratani.
Aliongeza kuwa Wakenya wengi hupuuzilia mbali suala la kujua hali zao za kiafya, jambo linalopelekea mtu kuugua bila kujua, hadi saratani inapofika hatua mbaya.
Aidha, alidokeza kuwa kituo hicho hupokea zaidi ya wagonjwa 30 kila mwezi, ishara tosha kuwa ugonjwa wa saratani ni miongoni mwa magonjwa yanayosababisha maafa nchini.
Vile vile, alisema saratani ya kizazi inaongoza hapa Mombasa ikifuatiwa na ile ya matiti ambayo hushika pia wanaume.
Aliwasihi wananchi kutembelea vituo vya afya ilikujua hali zao za kiafya, kama njia moja ya kuepuka maradhi mbalimbali.