Vijana katika maeneo ya Kisauni, Nyali, Likoni na Changamwe wamehimizwa kujitenga na uhalifu unaodidimiza nia ya kufanikisha malengo yao na badala yake kujihusisha na miradi mbalimbali ya kuleta maendeleo mashinani.
Akizungumza katika eneo la Mtopanga eneo bunge la Kisauni siku ya Ijumaa, mfanyibiashara mashuhuri mjini Mombasa, Ali Mbogo, alisema kuwa ni jukumu la kila kijana kufikiria maswala muhimu ya kujijenga kimaendeleo na kujitenga na uhalifu ili ndoto zao zifaulu.
Mbogo ambaye pia ni mgombea wa kiti cha eneo bunge hilo katika uchaguzi mkuu ujao, alisema kuwa vijana ndio watakaoijenga taifa la Kenya kimaendeleo na lazima wajitenge na visa vya uhalifu na badala yake kudumisha amani.
“Vijana tafadhali tunawaomba mujitenge na maswala ya kihalifu ambayo hayatawasaidia katika kufanikisha ndoto zenu. Uhalifu utawapelekea kukabiliwa na maafisa wa usalama na kujeruhiwa kila uchao. Sisi kama viongozi tuko na mpango wa kuwasaidia kubadilika kimaisha na kuweka amani mashinani na kukuza uchumi wa nchi,” alisema Mbogo.
Mbogo aliwarai wakaazi wa eneo la Mtopanga na eneo bunge la Kisauni kwa jumla kumchagua kama kiongozi wa eneo bunge hilo katika uchaguzi mkuu ujao.