Padri wa jimbo katoliki la Nakuru amewahimiza vijana ambao wamejiiingiza katika makundi haramu kubadili mienendo yao.
Akihubiri siku ya Jumanne katika eneo la Kikapu kwenye ibaada ya misa ya wafu ya mmoja wa vijana walioaga dunia katika ajali ya barabarani iliyofanyika katika eneo la Salgaa mkesha wa mwaka mpya, Padri Bethwel Mwaura alisema kuwa vijana bado wana nafasi ya kubadili mienendo yao.
Padri huyo alisema vijana hao wanaweza kushauriwa na vijana wenzao walio katika makundi ya vijana, wanaotoa ushauri nasaha.
Alisema kuwa ni rahisi kwa vijana waliojiunga na makundi hayo kuzungumza na kushauriana na wenzao.
Wakati huo huo, amewahimiza vijana kutoshawishiwa kujiunga katika makundi yasiyo na mienendo mizuri.
“Kwa kufuata mienendo mizuri na kujihusha na makundi yenye maadili mema, vijana watakuwa na maisha mazuri katika siku za usoni. Ningependa kuwahimiza Wakenya kuwaombea vijana kwani hao ndio viongozi na tegemeo la kesho hapa nchini,” alisema Mwaura.
Kwa upande mwingine, ametaka viongozi kwenye Kaunti ya Nakuru na hapa nchini kwa jumla kuchukua hatua zifaazo kuzuia maafa ya barabarani badala ya kusubiri hadi vifo vitokee ili hatua hizo ziweze kuchukuliwa.