Hazina ya Uwezo Fund katika eneo bunge la Nyaribari Chache, Kaunti ya Kisii, imepokeza vyama 120 vya vijana mikopo ya kuanzisha biashara ili kujiimarisha na kujiendeleza kimaisha.
Kila chama kilipokea mkopo wa shillingi 50,000 ili kuanza biashara kama njia moja ya kujikimu kimaisha, huku wakitakiwa kujiendeleza badala ya kutegemea watu wengine.
Akizungumza siku ya Jumatano katika eneo la Kiogoro wakati alipopokeza vikundi hivyo mikopo hiyo, mwenyekiti wa hazina hiyo katika eneo bunge hilo Josephat Nyamache, aliomba vikundi hivyo kutumia pesa hizo vizuri kwa kuanza biashara.
kulingana na Nyamache, vikundi hivyo vitarudisha pesa hizo baada ya miezi misita ili kupokezwa zingine ikiwa wanahitaji kuongezewa.
“Hazina ya uwezo katika eneo bunge hili imeonekana kunufaisha wengi kwa kuwawezesha kujiendeleza kupitia biashara ambazo huleta faida,” alisema Nyamache.
Aidha, Nyamache aliomba vikundi hivyo kuhakikisha vimerudisha pesa hizo baada ya miezi sita, ili kupata fursa ya kupokezwa zingine.
“Mwaka jana hazina hii ya uwezo ilitoa millioni tisa kwa vikundi hivyo lakini ni vichache ambavyo vilirudisha pesa hizo,” alisema Nyamache
Aliongeza, “Naomba vikundi vile ambavyo havijarudisha pesa baada ya muda waliowekewa kukamilika wafanye hivyo ili pesa hizo ziweze kusaidia wengine.”