Huku taifa likizidi kushuhudia changamoto si haba,wito umetolewa kwa viongozi wa kidini kuhakikisha kwamba wanatoa mwelekeo kwa baadhi ya changamoto.
Mchungaji Daniel Guchu amesema kuwa kanisa halifai kuwa kimya wakati maovu yanatendeka.
Akizungumza wakati wa ibada ya Jumapili katika kanisa la PCEA Dr. Arthur, mchungaji Guchu alisema kuwa baadhi ya matatizo yanayokumba taifa ni kutokana na hatua ya baadhi ya viongozi wa kidini kufeli.
"Kuna changamoto nyingi sana katika taifa hili, na viongozi wa kidini wanafaa kujitokeza na kusaidia kutatua," alisema Guchu.
Isitoshe, amedokeza kuwa kanisa pia lina changamoto miongoni mwa viongozi na huenda ndio sababu kuu ya serikali kujaribu kudhibiti makanisa.
"Baadhi ya hizi changamoto na ukosefu wa mwelekeo ndio ulipelekea serikali kuleta sheria za kudhibiti makanisa," aliongeza Guchu.
Amewashtumu vikali baadhi ya wachungaji laghai akisema wanachafua injili ya mwenyezi Mungu.