Wanasiasa wa mrengo wa Cord waliohamia vyama vingine wamesutwa vikali na wenzao waliokutana na kiongozi wa muungano huo Raila Odinga, alipozuru Mombasa siku ya Jumatano.
Wanasiasa hao ambao baadhi ya walitangaza wazi kuhama Cord na kujiunga na upande wa serikali, wametajwa kama wasaliti na wasio na msimamo dhabiti wa kuendesha vyama, na kuleta maendeleo kwa watu wanaowawakilisha.
Akizugumza mjini Mombasa, mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Kilifi Bi Aisha Jumwa, alimtaja mbunge wa Kilifi Kaskazini Gideon Mung’aro, pamoja na yule wa Lungalunga Khatibu Mwashetani, kama walipoteza mwelekeo.
“Mung’aro anatuaibisha kama chama pamoja na watu wa Malindi kwa ujumla. Sisi hatuwezi kujivunia na Jubilee kivyovyote kwa sababu hata hatuna mwakilishi wetu huko. Mimi hao nawaona kama wasaliti wakubwa,” alisema Jumwa.
Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi kwa upande wake aliwaonya wale wote wenye nia ya kuhama muungano wa Cord, kwa kusema kwamba hawatapata kura kutoka kwa Wapwani, na uamuzi wao utawakosesha nafasi kuingia bungeni.
“Mimi nawaambia mapema.Kkama wewe umeamua kuingia Jubilee basi usahau kuingia bunge kwa sababu hapa utaanguka patupu,” alisema Mwinyi.