Huku ziara ya Rais Uhuru Kenyatta ikiendelea katika eneo la Pwani, joto la kisiasa bado linaendelea kushuhudiwa huku viongozi mbalimbali wakionekana kutofautiana hadharani.
Wakati wa afla ya kupeana hati miliki kwa maskwota wa shamba la Waitiki wilayani Likoni wiki chache zilizopita, malumbano yalishuhudiwa baina ya Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho na Seneta wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko.
Katika zoezi hilo lililoongozwa na Rais Kenyatta, Sonko alitoa matamshi makali dhidi ya wakaazi wa Mombasa huku akiwaambia kuwa lazima wamheshimu rais na kwamba hatokubali kuona mtu yeyote akimdharau.
“Ningependa kukwambia Bwana Sonko kwamba sisi watu wa Mombasa ni wangwana na wala hatujibu kwa matusi,” Joho alimjibu seneta Sonko.
Uhasama wa viongozi hao haukuishia hapo. Walikutana tena siku ya Ijumaa katika uwanja wa Makadara Grounds wakati rais alipokuwa akizindua mradi wa 'Mwangaza Mtaani'.
Huku hayo yakijiri, seneta wa Mombasa Hassan Omar hajaonekana katika mikutano ambayo rais amekuwa akifanya katika eneo hilo.
Hatua hiyo imezua maswali miongoni mwa wananchi, huku wakijiuliza iwapo anaunga mkono miradi inayoendeshwa na serikali.
Seneta huyo alivunja kimya chake kwa kutoa matamshi yaliyoonyesha wazi kwamba hakubaliani na mradi wa 'Mwangaza Mtaani' ulioanzishwa na Rais Kenyatta siku ya Ijumaa.
Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumamosi siku moja baada ya uzinduzi huo, Omar aliitaka serikali kuzingatia zaidi kuimarishwa kwa usalama katika eneo hilo.
“Ukitembea eneo hili wakati wa usiku utapata kwamba hakuna watu na hii inatokana na ukosefu wa usalama. Serikali inafaa kuzingatia swala la usalama kwanza kabla ya kuanzisha mradi huu,” alisema Seneta Omar.