Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Baadhi ya wenyeji katika mtaa wa Kibuyuni B eneo bunge la Likoni wametoa wasiwasi wao kuhusiana na visa vya kuibiwa kwa mifugo wao hasa kuku na vijana wanawashuku kuwa 'Mateja'. 

Kulingana na mama Mwanahamisi Halima ambaye aliongea kwa niaba ya wakazi siku ya Jumatatu, alisema kuwa vijana wengi wamejihusisha na wizi wa kuku pamoja na vitu vingine vya kubebeka vya nyumbani.

Hali hii ambayo wakazi hao wanadai kusababishwa na kujiondoa kwa vijana wengi katika mpango wa urekebishaji tabia ulioanzishwa chini ya mpango wa serikali kuu kwa ushirikaiano na serikali za kaunti za maeneo yote yanayoathiriwa na matumizi ya dawa za kulevya.

Mmoja wa wazazi hao ambaye hakutaka kutajwa aliwalaumu baadhi ya wazazi wa vijana hao kwa kuonekana kuwatetea watoto wao hata wanapopatikana mali ya kuiba. 

Wazazi hao wametaka jamii ya eneo hilo kuchangamkia malezi ya wanao vilivyo na kuonya kuwa huenda wengine wakajipata katika hali ya majuto.

Vijana hao mara nyingi hujihusisha na kuomba pesa kutoka kwa wazazi hao na wanapokosa kupewa hela hizo hujikita katika patashika za kuiba na hata kuwaotea watu njiani wanapotoka kazini na kuwaibia chochote walicho nacho.