Share news tips with us here at Hivisasa

Idadi ndogo ya watu ilishuhudiwa kwenye baadhi ya vituo vya kusajili wapiga kura katika Kaunti ya Mombasa baada ya zoezi hilo kuanza rasmi siku ya Jumatatu.

Huku tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC ikiendelea kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa usajili huo, ni wakaazi wachache mno walioonekana kuchangamkia zoezi hilo.

Akiongea na mwandishi huyu katika kituo cha usajili cha Makadara Grounds mjini humo, Luthman Nasir, mmoja wa wasajili alisema kuwa walilazimika kuanza shughuli hiyo kwa kuchelewa kufuatia ukosefu wa umeme.

Nasir alisema kuwa changamoto ingine ni watu kutoelewa sehemu maalum ambapo vituo hivyo vimewekwa kuhudumia wananchi.

“Watu wengi hawajui mahali ambapo hivi vituo vilipo, na hiyo ni mojawapo ya sababu ya watu wachache kushuhudiwa katika siku za mwanzo,” alisema Nasir.

Kwa upande wao, wananchi waliojisajili walielezea umuhimu wa kujitokeza siku za , wakiongeza kuwa hatua hiyo itapunguza msongamano.

“Mimi nimekuja leo kwa sababu uwa niko na shughuli nyingi na singependa kungoja hadi ile siku ya mwisho ambapo watu watakuwa wengi,” alisema Amos Owino, mkaazi.

Hata hivyo, maafisa wa usajili katika vituo hivyo wamewahimiza wananchi kujitokeza mapema badala ya kungojea hadi pale muda unapokamilika.

Zoezi la usajili wa wapiga kura lilianza rasmi siku ya Jumatatu kote nchini huku likitarajiwa kukamilika tarehe 15 mwezi Machi, ambapo unaendeshwa katika kata 1, 450 kote nchini.

Wakati huo huo, viongozi wa kisiasa nchini wanaendelea kuhimiza Wakenya kujisajili kwa wingi kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017 ili wapate fursa ya kushiriki katika uchaguzi huo.