Share news tips with us here at Hivisasa

Washikadau katika sekta ya hoteli eneo la Pwani wameunga mkono hatua ya Waziri wa Utalii Najib Balala ya kupunguza gaharama ya usafiri wa anga kwa watalii wanaozuru eneo hilo ili kuimarisha sekta hiyo.

Waziri huyo ambaye alitoa tangazo hilo siku ya Alhamisi, alisema kuwa moja kati ya sababu zinazopelekea idadi ya watalii wanaozuru Pwani kupungua ni gharama ya juu ya usafiri.

Akiongea na mwandishi huyu siku ya Ijumaa mjini Mombasa, mkurugenzi wa chama cha wamiliki wa hoteli Pwani Sam Ikwaye, alisema wameipokea vyema hatua ya Waziri Balala na kwamba wana matumaini kwamba italeta mabadiliko.

“Hilo ni jambo ambalo kama washikadau tunaliunga mkono na tuna matumaini ifikiapo mwaka ujao, mambo yatakuwa yamebadilika,” alisema Ikwaye.

Mkurenzi huyo alisema kuwa swala la usafiri wa watalii hadi eneo hilo limekuwa changamoto kubwa licha ya kwamba ni eneo lenye maeneo mbalimbali ya kuvutia.

Takwimu kutoka kwa Wizara ya Utalii nchini inaonyesha kuwa eneo la Pwani huchangia asilimia 60 ya mapato kutoka kwa sekta hiyo, huku Mombasa ikongoza miongoni mwa kaunti za Pwani.

Punguzo hilo la gharama ya usafiri kwa watalii linalenga ndege zinazozuru kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Moi mjini Mombasa, na kile cha Malindi ambavyo ndivyo viwanja vikuu vinavyopokea ndege kutoka mataifa ya nje.