Wafanyibiashara mjini Nyamira wametakiwa kuasi tabia ya kufanya maandamano ya mara kwa mara wakilalamikia kulipa leseni za kufanya biashara.
Akihutubia baadhi ya wafanyabiashara hao mjini Nyamira, mwakilishi wadi ya Nyamira mjini Robert Ongwano alisema kuwa yafaa wafanyibiashara hao kushiriki mazungumzo na serikali ya kaunti hiyo badala ya kuandamana.
Alisema kuwa kupitia kwa mazungumzo serikali inaweza kusikiza matakwa yao na kisha kuwahudumia vyema.
"Badala yenu kushiriki maandamano kila mara mnapo hitajika na serikali ya kaunti kulipia leseni zenu za biashara, ingelikuwa vizuri mngeiteua kamati itakayoketi pamoja na serikali ili kuwasilisha matakwa yenu kwa njia inayostahili. Majadiliano yataiwezesha serikali kuwahudumia vizuri," alisema Ongwano.
Mwakilishi huyo aidha aliongeza kwa kusema kuwa Wakenya wana haki ya kutoa maoni kuhusiana na viwango vya ushuru wanavyo stahili kulipa, ili kupokea leseni za kuwawezesha kuendesha biashara mbalimbali kupitia kwa kufanya mazungumzo na serikali.
"Ninajua kuwa kila mara mswada wa kiwango cha pesa wanacho stahili kutozwa wananchi unapojadiliwa, watu wengi huona kuwa serikali ndiyo inayo wakosea. Bunge la kaunti kupitia kwa wawakilishi wadi na pia wananchi huhusishwa kabla ya mswada huo kupitishwa, kwa maana kupitia majadiliano hayo, wananchi hupewa nafasi ya kuwasilisha mapendekezo yao," alisema Ongwano.